Thursday, September 25, 2014

Fadhila Za Siku Ya 'Arafah Na Yawmun-Nahr (Siku Ya Kuchinja)




‘Arafah ni jabali ambalo alisimama Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwahutubia Maswahaba alipotekeleza Hijja ya kuaga. Na hapo ndipo wanaposimama Mahujaji kutimiza kilele cha ‘Ibaadah hii ya fardhi. Kusimama hapo ndio nguzo mojawapo kuu ya Hijjah bila ya kuweko hapo mwenye kuhiji atakuwa hakutimiza hijja yake kutokana na dalili  ifuatayo:

عن عبد الرحمن بن يعمر قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم:  ((الْحَجُّ عَرَفَة ، مَنْ جَاءَ قَبْلَ طُلُوعِ الْفَجْرِ مِنْ لَيْلَةِ جَمْعٍ فَقَدْ أَدْرَكَ الْحَجّ))  صحيح الجامع   

Kutoka kwa ‘Abdur-Rahmaan bin Ya’mur ambaye amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Al-Hajj ni ‘Arafah, atakayekuja kabla kutoka Alfajiri usiku wa kujumuika atakuwa ameipata Hajj)) [Swahiyh Al-Jaami’].


Fadhila Za Siku ya ‘Arafah:


1-Ni Siku Iliyokamilika Dini Yetu  

قال رجل من اليهود لعمر : يا أمير المؤمنين ، لو أن علينا نزلت هذه الآية : ((اليوم أكملت لكم دينكم وأتممت عليكم نعمتي ورضيت لكم الإسلام دينا)) لاتخذنا ذلك اليوم عيدا ، فقال عمر: "إني لأعلم أي يوم نزلت هذه الآية ، نزلت يوم عرفة ، في يوم جمعة"  البخاري

Kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Myahudi mmoja alimwambia: “Ewe Amiri wa Waumini, lau ingeliteremka kwetu sisi Aayah hii ((Leo Nimekukamilishieni Dini yenu na Nimekutimzieni Neema Zangu kwenu na Nimekuridhieni Uislamu kuwa ni Diyn yenu)) [Al-Maaidah (5: 3] tungeliifanya ‘Iyd siku hiyo. Akasema ‘Umar: “Hakika naijua siku gani imeteremka Aayah hii. Imeteremka Siku ya ‘Arafah siku ya Ijumaa” [Al-Bukhaariy)


Na ukamilifu wa dini siku hiyo ni kwa vile Waislamu hawakupata kutekeleza Hajj kabla ya hapo ya Kiislamu. Na kukamilika dini yao ni kukamilisha nguzo za Kiislamu zote.  


2-Kufunga Swawm ni kufutiwa madhambi ya miaka miwili:

Ni fadhila kubwa kwetu kujitakasa na madhambi tunayoyachuma kila siku kwani binaadamu daima ni mkosa.


عَنْ أَبِي قَتَادَةَ رضي الله عنه أن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ :  ((صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ )) أخرجه مسلم

Imetoka kwa Abu Qataadah (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Swawm ya 'Arafah nataraji (kwa Allaah) kufuta madhambi ya mwaka uliopita na wa baada yake.” [Muslim]

Umuhimu huo wa kufunga na msisitizo ni kwa wasiohiji, na walio katika Hajj wao hakuna msisitizo huo kwa dalili ifuatayo:

عن ميمونة بنت الحارث: أن الناس شكوا في صيام النبي صلى الله عليه وسلم يوم عرفة ، فأرسلت إليه بحلاب ، وهو واقف في الموقف ، فشرب منه والناس ينظرون" البخاري

Kutoka kwa Maymuunah bint Al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anhaa) kwamba watu walitia shaka na Swawm ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa  aalihi wa sallam) [kama alifunga] Siku ya ‘Arafah, nikampelekea maziwa, naye akiwa amesimama akayanywa na huku watu wanamtazama.”  [Al-Bukhaariy]



3-Ni Siku Bora Kabisa Ambayo Wataokolewa Waja Kutokana Na Moto; Wataghufuriwa Madhambi Yao



عن  جابر  رضي الله عنه  عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((مَا مِنْ يَوْمٍ أَفْضَلُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ يَوْمِ عَرَفَةَ، يَنْزِلُ اللَّهُ تَعَالَى إلَى سَمَاءِ الدُّنْيَا فَيُبَاهِي بِأَهْلِ الْأَرْضِ أَهْلَ السَّمَاءِ)) وروى ابن حبان
وفي رواية: ((إنَّ اللَّهَ يُبَاهِي بِأَهْلِ عَرَفَةَ مَلَائِكَتَهُ، فَيَقُولُ: يَا مَلَائِكَتِي، اُنْظُرُوا إلَى عِبَادِي، قَدْ أَتَوْنِي شُعْثا غُبْرا ضَاحِينَ))

Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa  aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna siku iliyo bora kabisa mbele ya Allaah kama siku ya ‘Arafah. Anateremka Allaah Ta’ala mbingu ya dunia (ya kwanza) kisha Anawafakhiri watu  ardhi  kwa watu wa mbingu.”


Na katika riwaaya nyingine: “Hakika Allaah Anawafakhiri watu ‘Arafah kwa Malaika Wake. Husema Husema Ee Malaika wangu, watazameni waja Wangu wamenijia wakiwa timtimu wamejaa vumbi …”

Pia,

 عن عائشة  رضي الله عنها عن النبي صلى الله عليه وسلم: ((ما من يوم أكثر من أن يعتق الله فيه عبيدا من النار من يوم عرفة ، وأنه ليدنو ، ثم يباهي بهم الملائكة فيقول : ما أراد هؤلاء ؟ اشهدوا ملائكتي أني قد غفرت لهم )) صحيح الترغيب

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakuna siku Anayoacha Allaah kwa wingi huru waja kutokana na moto kama siku ya ‘Arafah. Na huwa karibu kisha Anajigamba kwao kwa Malaika na Husema: Wametaka nini hawa? Shuhudieni Malaika wangu kwamba hakika Mimi Nimewaghufuria)) [Swahiyh At-Targhiyb]
  

عن جابر  رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم-(( ما من أيام عند الله أفضل من عشر ذي الحجة قال فقال رجل يا رسول الله هن أفضل أم عدتهن جهادا في سبيل الله قال: (( هن أفضل من عدتهن جهادا في سبيل الله وما من يوم أفضل عند الله من يوم عرفة ينزل الله تبارك وتعالى إلى السماء الدنيا فيباهي بأهل الأرض أهل السماء فيقول انظروا إلى عبادي جاءوني شعثا غبرا ضاحين جاءوا من كل فج عميق يرجون رحمتي ولم يروا عذابي فلم ير يوم أكثر عتيقا من النار من يوم عرفة))   الترغيب والترهيب - إسناده صحيح أو حسن 

Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna Siku iliyo bora kabisa kama siku kumi za Dhul-Hijjah, akasema mtu: “Ee Mjumbe wa Allaah, hizo ni bora au Jihaadi katika njia ya Allaah? Akasema: “Hizo ni bora kuliko Jihaad katika njia ya Allaah, na hakuna siku bora kabisa mbele ya Allaah, kama siku ya ‘Arafah, Anateremka Allaah Tabaaraka wa Ta’ala katika mbingu ya dunia kisha Anawafakhiri watu wa ardhini kwa watu wa mbinguni kisha Anasema: Tazameni waja Wangu wamenijia timtimu wamejaa vumbi wamekuja kutoka kila pembe ya mbali wanataraji Rehma Yangu na wala hawajaona adhabu Yangu. Na wala hakuona siku inayoachwa huru shingo kutokana na moto kama siku ya ‘Arafah.” [At-Targhiyb wat-Tarhiyb – Isnaad yake Swahiyh au Hasan]
  
  
4.    Siku Ya Kutakabaliwa Du’aa

Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa  aalihi wa sallam):

 ((خير الدعاء دعاء يوم عرفة، وخير ما قلت أنا والنبيون من قبلي: لا إله إلا الله وحده لا شريك له، له الملك وله الحمد وهو على كل شيء قدير)) روى الترمذي
  
“Du’aa bora kabisa ni du’aa katika siku ya 'Arafah, na yaliyo bora kabisa niliyosema mimi na Mitume kabla yangu ni: 'Laa Ilaaha Illa Allaah Wah-dahu Laa Shariyka Lahu, Lahul-Mulku Wa-Lahul-hamdu Wa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr – Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah, Pekee Hana mshirika, ufalme wote ni Wake, na Sifa njema zote ni Zake, Naye ni Mweza wa kila kitu daima.” [At-Tirmidhiy]




6-     Siku Ambayo Allaah Ameiapia

Allaah Ameiapia siku hii ya ‘Arafah ambayo inajulikana kwa ‘Siku ya Kushuhudiwa’. Hii kutokana na kauli Yake Subhaanahu wa Ta’ala:
بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ  ((وَالسَّمَاء ذَاتِ الْبُرُوجِ))  (( وَالْيَوْمِ الْمَوْعُودِ))   ((وَشَاهِدٍ وَمَشْهُودٍ))
((Naapa kwa mbingu yenye Buruji!))  ((Na kwa siku iliyoahidiwa!)) ((Na kwa shahidi na kinachoshuhudiwa!)) [Al-Buruuj 85: 1-3]

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: “Siku ya kuahidiwa ni siku ya kufufuliwa. Siku ya kushuhudiwa ni siku ya ‘Arafah, na Siku ya kinachoshuhudiwa ni Siku ya Ijumaa)) [At-Tirmidhiy na imepewa daraja ya Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]

7-Siku Ambayo Allaah Amechukua Fungamano (ahadi) Kutoka Kizazi Cha Aadam

Imesimuliwa kwamba Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: “Allaah Amechukua fungamano kutoka mgongo wa Aadam katika Na’maan yaani ‘Arafah. Akalete mbele mgongo wake kizazi chake chote na akawatandaza mbele Yake.. Kisha Akawakabali kuwauliza:
 ((أَلَسْتَ بِرَبِّكُمْ قَالُواْ بَلَى شَهِدْنَا أَن تَقُولُواْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَذَا غَافِلِينَ)) (( أَوْ تَقُولُواْ إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِن قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً مِّن بَعْدِهِمْ أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ))
((Je, Mimi si Mola wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia. Msije mkasema Siku ya Qiyaamah sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo)) ((Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walioshirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi Utatuangamiza kwa sababu ya waliyoyafanya wapotovu?)) [Al-A’araaf 7: 172-173] [Imesimuliwa na Ahmad na imepewa daraja ya Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]


Kutokana na fadhila hizo, ndio ikawa ni siku tukufu kabisa na siku ambayo ruknu ya Hajj kuu inatimizwa na bila ya mtu kusimama ‘Arafah inakuwa hakutekeleza Hajj.

Fadhila Za Yawmun-Nahr – Siku ya Kuchinja:
Siku kuu ya ‘Iydul-Adhw-haa na ndio inajulikana pia kwa Yawmun-Nahr.

Kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): 

((إن أعظم الأيام عند الله يوم النحر، ثم يوم الق))  أبي داود

“Siku iliyo tukufu kabisa kwa Allaah ni siku ya kuchinja, kisha siku ya kutulia”  (yaani siku ya kukaa Mina)  [Abu Daawuud]
Sababu ya kuchinja ni kufuata Sunnah ya baba yetu Nabii ‘Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) alipotaka kumchinja mwanawe Ismaa’iyl na Allaah Akamteremshia badala yake kafara ya mnyama.

Kuchinja - Fadhila, Hikmah Na Hukmu Zake


Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala):
((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))
((Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako)) [Al-Kawthar: 2]
Kuchinja ni moja ya ibada za Kiislam ambayo inatukumbusha Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Baraka Zake kwetu, pamoja na kutupa mafunzo ya utiifu wa baba yetu Ibraahiym kwa Mola wake na kumpwekesha Allaah. Hivyo ibada hii ya kuchinja ni muhimu sana kwa Muislam, na inatupasa tuizingatie kwa makini na kuitekeleza.
UBAINIFU WAKE
Ni kuchinja kondoo, ngamia au ng'ombe siku ya 'Iydul-Adhwhaa na siku za Tashriyq (siku ya 11, 12, 13 Dhul-Hijjah) ili kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).
KUWAJIBIKA KWAKE
Kuchinja ni waajib katika familia ya kila nyumba ya Muislamu, ambayo watu wake wanao uwezo wa kuchinja. Hii kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))
((Basi Swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako)) [Al-Kawthar: 2]
 ((وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ))
((Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Allaah; kwa hao mna kheri nyingi)) [Al-Hajj: 36]
Na uthibitisho wa Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
 (( ضحى بكبشين أملحين أقرنين ذبحهما بيده وسمى وكبر)) رواه البخاري ومسلم 
((Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja kondoo wawili walionona, walio na pembe, aliwachinja kwa mikono yake akataja jina la Allaah, Akamtukuza kwa kusema BimiLLaah Allaahu Akbar)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Aliulizwa Shaykh Muhammad bin 'Uthaymiyn kama masikini inampasa achinje. Akajibu "Ikiwa anao uwezo wa kuchinja basi achinje ili apate kheri hizi na kama hana uwezo basi haimpasi" 
Maoni ya wanachuoni wengi kuhusu Fadhila, Hukmu na Hekima za Hajj ni kama yafuatayo:
FADHILA ZAKE
Kuna ushahidi kwamba ibada ya kuchinja ina fadhila kubwa kwa sababu ya kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
 عن عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((ما عمل ابن آدم يوم النحر عملاً أحبُّ إلى الله من إراقة الدم، وإنه ليؤتى يوم القيامة بقرونها، وأظلافها، وأشعارها، وإن الدم ليقع من الله عز وجل بمكان قبل أن يقع على الأرض، فطيبوا بها نفساً))
Kutoka kwa mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu anhaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna kitendo cha mwana Adam kilichokuwa ni kipenzi kabisa kwa Allaah siku ya kuchinja kama kumwaga  damu (kuchinja). Atakuja (huyo mnyama) siku ya Qiyaamah na pembe zake, kucha zake na nywele zake. Damu yake itamwagika mahali fulani Allaah Anapajua kabla ya kumwagika katika ardhi. Hivyo zipendezesheni nafsi kwayo)) [At-Tirmidhiy]
HIKMAH YAKE
1.    Kujikurubisha Kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama Anavyosema katika kauli Yake: 
((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))
((Basi Swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako)) [Al-Kawthar: 2]
Anasema pia:
((قُلْ إِنَّ صَلاَتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ))
 (( لاَ شَرِيكَ لَهُ وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَاْ أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ))
((Sema: Hakika Swalah yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Allaah Mola wa viumbe vyote)) 
((Hana mshirika Wake. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu)) [Al-An'aam: 162-163]. 
((لَن يَنَالَ اللَّهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَكِن يَنَالُهُ التَّقْوَى مِنكُمْ كَذَلِكَ سَخَّرَهَا  لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ))
        
((Nyama zao hazimfikii Allaah wala damu zao, lakini unamfikia uchaji Allaah wenu. Namna hivi Tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Allaah kwa Alivyokuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema)) [Al-Hajj: 37].
Na kafara ni kuchinja kwa kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
2.    Kuihuiisha Sunnah Mojawapo Ya Tawhiyd, wakati Allaah Alipompa wahyi Ibraahiym (alayhis-salaam) amchinje mwanawe Ismaa'iyl. Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akampa fidia ya kondoo, akamchinja badala yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
((وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ))
((Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu)) [Aswaaffaat: 107]          
3.    Muislam Kuweza Kuwalisha Nyama Familia Yake Pamoja Na Jamaa Zake Siku Ya 'Iyd na kueneza Rahma miongoni mwa masikini na mafakiri.
 
4.    Kutoa Shukurani Kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  kutujaalia kuwa na wanyama wafugwao kama Anavyosema:
((وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ كَذَلِكَ سَخَّرْنَاهَا لَكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ))
 (( لَن يَنَالَ اللَّهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَكِن يَنَالُهُ التَّقْوَى مِنكُمْ كَذَلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ))
((Na ngamia wa sadaka Tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Allaah; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Allaah juu yao wanaposimama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na walisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba. Ndio kama hivi Tumewafanya hawa wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru))
((Nyama zao hazimfikii Allaah wala damu zao, lakini unamfikia uchaji Allaah wenu. Namna hivi Tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Allaah kwa Alivyokuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema)) [Al-Hajj: 36-37]
HUKMU ZAKE
Umri Wake:                            
Kondoo wawe ni kondoo jike ambao wamekamilisha umri wa mwaka mmoja takriban. Mbuzi wawe wamekamilisha umri wa mwaka mmoja na kuingia mwaka wa pili. Ngamia wawe wamekamilisha umri wa miaka minne na kuingia wa tano. Ng'ombe wawe wamekamilisha miaka miwili na kuingia mwaka wa tatu, kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((لا تذبحوا إلا مسنة إلا أن تعسر عليكم فتذبحوا جذعة من الضأن)) رواه مسلم
((Msichinjie ila mnyama mwenye makamo isipokuwa ikiwa ni shida kwenu, hivyo mchinje kondoo (japo wa chini ya umri wa mwaka lakini awe zaidi ya umri wa miezi sita)) [Muslim] 
Usalama Wake:
Asiwe na kasoro yoyote kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi   wa aalihi wa sallam) amesema:
((أربع لا تجوز في الأضاحي: العوراء  البيّن عورها، والمريضة البيّن مرضها،  والعرجاء  البيّن ظلعها ،  والعجفاء  التي لا تنقي))  
((Mambo manne (kasoro nne) hayapasi katika kuchinja; mwenye jicho chongo lenye kudhihirika, mnyama mgonjwa mwenye kudhihirika ugonjwa wake, kilema mwenye kudhihirika kuchechemea kwake na aliyedhoofika ambaye hana nyama katika mifupa yake)) [Swahiyh Al-Jaami']  
Wakati Wa Kuchinja:
Kuchinja asubuhi ya siku ya 'Iyd baada ya Swalah. Hairuhusiwi kuchinja kabla ya Swalah kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
حديث أنس  رضي الله عنه- قال: قال رسول الله -صلى الله عليه وسلم  ((من ذبح قبل الصلاة فإنما ذبح لنفسه، ومن ذبح بعد الصلاة فقد تم نسكه وأصاب سنة المسلمين)) البخاري ومسلم
Kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu 'anhu kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayechinja kabla ya Swalah atakuwa amejichinjia kwa ajili yake mwenyewe. Na Atakayechinja baada ya Swalah atakamilisha kafara (kichinjo) yake na atapata   (atatekeleza) Sunnah ya Waislam)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Anaweza kuchinja siku ya pili ya 'Iyd au kuchelewesha hadi siku ya mwisho ya Ayyaamut-Tashriyq (siku za Tashriyq) ambayo ni siku ya kumi na tatu Dhul-Hijjah.           
  (... وفي كل أيام التشريق ذبح))  
((...siku zote za Tashriyq ni siku za kuchinja)) [Ahmad]
YANAYOPENDEKEZEKA KATIKA KUCHINJA 
Kumpwekesha Allaah:
Inapendekezeka kumuelekeza mnyama Qiblah wakati wa kumchinja na kusoma:
 ((إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ حَنِيفًا وَمَا أَنَاْ مِنَ الْمُشْرِكِينَ)) 
((Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa Aliyeziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina))[Al-An'aam:79]
((إِنَّ صَلاَتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ))     ((لاَ شَرِيكَ لَهُ وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَاْ أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ))
((Hakika Swalah yangu, na kichinjo changu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Allaah, Mola wa viumbe vyote)) 
((Hana mshirika Wake. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu)) [Al-An'aam: 162-163]. 
Anapoanza Kuchinja Aseme:
((بسم الله والله اكبر، اللهم هذا منك ولك))
((BismiLLaah, wa Allaahu Akbar, Ewe Allaah hii ni kutoka Kwako na kwa ajili Yako))
Kuchinja mwenyewe ni bora zaidi:
Inapendekezeka Muislamu achinje mwenyewe na akimuwakilisha mtu kumchinjia pia inaruhusiwa hakuna ikhtilaaf katika jambo hili baina ya Maulamaa.   
KUGAWA NYAMA  
Inapendekeza kuigawa nyama sehemu tatu. Ya kwanza wale familia yake, sehemu ya pili kugawa sadaqah na sehemu ya tatu kuwagawia marafiki, jirani n.k. kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَى مَا رَزَقَهُم مِّن  بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ))
((Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Allaah katika siku maalumu juu ya nyama hao Aliowaruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri)) [Al-Hajj: 28]
((وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ))
((Na ngamia wa sadaka Tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Allaah, kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Allaah juu yao wanaposimama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na walisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba)) [al-Hajj: 36]
Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
((كلوا وأطعموا وادخروا)). رواه البخاري
((Kuleni, lisheni na mbakishe [akiba])) [Al-Bukhaariy]
Na usemi mwengine kutoka kwa Muslim kutoka kwa mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa)
عن عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلّم قال: ((كلوا وادخروا وتصدقوا)) رواه مسلم.
 ((Kuleni, bakisheni na mtoe sadaka)) [Muslim]
Inaruhusiwa pia kuigawa nyama yote sadaqah na Inaruhusiwa kubakisha sehemu.  
HAIFAI KUMPA CHOCHOTE KATIKA NYAMA MCHINJAJI KAMA UJIRA
Hairuhusiwi kumlipa mchinjaji aliyewakilishwa kuchinja baadhi ya nyama kama ujira wake kutokana na Hadiyth ifuatayo: 
عن علي قال‏:‏ أمرني رسول الله صلى الله عليه وسلم أن أقوم على بدنه وأن  أتصدق بلحومها وجلدها وأجلتها ‏(‏وأجلتها‏:‏ أي لباسها الذي يقيها البرد‏. )  وأن لا أعطي الجزار منها شيئا، وقال‏:‏ نعطيه من عندنا‏.
Kutoka kwa 'Aliy (Radhiya Alalhu 'anhu):"Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliniamrisha kuchinja? Na kutoa nyama, ngozi na kile kinachomfunika kumhifadhi na baridi kuvitolea sadaqah na nisimpe chochote katika nyama hiyo. ((Tutampa kitu tulichonacho)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ufafanuzi Zaidi:
Ukichinja AL-HADYI, mchinjaji hapewi katika nyama alioichinja lakini anapewa ujira wake. AL-HADYI ni kuchinja na wewe upo katika Hajj.
Ukichinja UDHWHIYAH, mchinjaji anaweza akapewa katika nyama hiyo aliyoichinja kama sadaka ikiwa ni masikini, na atapewa pamoja na ujira wake. UDHWHIYAH ni kichinjo kwa wale wasiokuwa katika Hajj. Walio katika Hajj kichinjo kinaitwa AL-HADYI. 
MNYAMA MMOJA ANATOSHELEZA FAMILIA NZIMA
Kuchinja mnyama mmoja anatosheleza katika kila familia japo kama kuna watu wengi katika familia kutokana na kauli ya:
  أبي أيوب -رضي الله عنه- لما سئل: كيف كانت الضحايا على عهد رسول الله؟  فقال: "كان الرجل يضحي بالشاة عنه وعن أهل بيته"  (الترمذي)
Abu Ayyuub (Radhiya Allaahu 'anhu) alipoulizwa: "Uchinjaji ulikuwa vipi zama za Mjumbe wa Allaah?" Akajibu: "Mtu alikuwa anachinja kondoo mmoja kwa ajili yake na familia yake" [At-Trimidhiy]
YANAYOMPASA KUFANYA MWENYE KUTAKA KUCHINJA
Baada ya kutia Niya ya kuchinja, asikate mtu nywele wala kucha mpaka amalize kuchinja kama tulivyoamrishwa katika Hadiyth ifuatayo:
عن أم سلمة رضي الله عنها، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال:  (( إذا رأيتم هلال ذي الحجة وأراد أحدكـم أن يضحّي فليمسك عــن شعره وأظفاره))  ، وفي راوية (( فلا يأخذ من شعره ولا من أظفـاره حتى يضحّي  )) مسلم
Imetoka kwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu 'anhaa)    kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  ((Ukiandama mwezi wa Dhul-Hijjah na ikiwa  yuko anayetaka kuchinja basi azuie (asikate) nywele zake na kucha zake))
Na katika riwaya nyingine ((Asikate nywele wala kucha mpaka atakapomaliza kuchinja)) [Muslim na wengineo]
         
MWENYE UWEZO WA KUCHINJA ZAIDI YA MMOJA
Mwenye uwezo wa kuchinja zaidi ya mmoja na akipenda achinje kama alivyochinja Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya Ummah wa Kiislam wote. Hivyo Muislam asiye na uwezo wa kuchinja naye atapata fadhila hizi za kuchinja, naye mchinjaji atachuma thawabu za Waislam wote wasio na uwezo. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya hivyo:
وعن أبي رافع رضي الله عنه «أن النبي صلىالله عليه وسلّم كان يضحي  بكبشين أحدهما عنه وعن آله، والاخر عن أمته جميعاً»، رواه أحمد
Kutoka ka Abu Raafi' (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba:  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akichinja kondoo wawili; mmoja kwa ajili yake na familia yake na wa mwengine kwa ajili ya Ummah wake wote)) [Ahmad]
Kutoka kwa Jaabir kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akichinja kwa ajili ya Ummah akisema:
 (( بسم الله والله أكبر. اللهم هذا عني وعمن لم يضح من أمتي))  رواه أحمد وأبو داود والترمذي.
((BismiLLaah, wa Allaahu Akbar, Ee Allaah hii kwa ajili yangu na kwa ajili ya wasio na uwezo katika Ummah wangu)) [Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy]
Wa BiLLaahi at-Tawfiyq