Ushauri Muhimu Kwa Mahujaji
Imefasiriwa na Ummu 'Abdil-Wahaab
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلاَ رَفَثَ وَلاَ فُسُوقَ وَلاَ جِدَالَ فِي الْحَجِّ وَمَا تَفْعَلُواْ مِنْ خَيْرٍ يَعْلَمْهُ اللّهُ وَتَزَوَّدُواْ فَإِنَّ خَيْرَ الزَّادِ التَّقْوَى وَاتَّقُونِ يَا أُوْلِي الأَلْبَاب))
((Hijjah
ni miezi maalum. Na anayekusudia kufanya Hijjah katika (miezi) hiyo,
basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala
asibishane katika hiyo Hijjah. Na kheri yoyote mnayoifanya, Allah
Huijua. Na chukueni masurufu (ya kutumia njiani, msiombe). Na hakika
masurufu bora ni yale yanayomfanya mtu asiombe (kwa kuwa yanamtosha).
Na nicheni Mimi, enyi wenye akili.)) [Al Baqarah: 197]
Kumtambua Allah
Njia
bora ya kumridhisha Allah ni kuwa na msimamo wa makini juu Yake,
kumtambua pamoja na kumuogopa Yeye katika matendo na mazungumzo yako
yote.
Kuwa na 'Aqiydah Sahihi
Kila
Muislaam ni lazima aelewe ya kwamba ikiwa imani au 'Aqidah yake sio
madhubuti, Hijjah au ibada yake yoyote huwa haikubaliwi. Kwa hivyo daima
jaribu kurekebisha imani yako kwa kuuliza Maulamaa ambao wataweza
kukupa ushahidi kutoka kwenye Qur-aan na Hadithi za Mtume (Swalla Allahu
'alayhi wa aalihi wa sallam).
Niyyah Iliyotakasika
Mwenyezi
Mungu Mtukufu Halikubali jambo lolote ambalo halikuelekezwa Kwake Yeye
Pekee. Kwa hivyo, ni lazima uwe na moyo mkunjufu na niyyah iliyotakasika
kwa ajili ya kutekeleza Hijjah.
Uhakika wa Vitendo vya Ibada
Tendo
lolote halikubaliwi isipokuwa liwe limetendwa sawasawa, kama vile
ambavyo limefanywa na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
ambaye ameonya:
( من أحدث في أمرنا هذا ما ليس منه فهو رد) متفق عليه.
((Atakayezusha katika jambo yasiyokuwa (katika Dini) yetu basi litarudishwa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Uvumilivu
Ugumu wa utekelezaji ibada ya Hijjah unahitaji kila hujaji kuwa mvumilivu na kuwasamehe wenzake.
Kutubia
Fanya
jitihada kwa kadiri ya uwezo wako ili Hijjah yako iwe ni toba ya
madhambi yako yote. Toba hii inahitaji kudumishwa ili usije ukarudia
tena kutenda madhambi.
Huruma
Fanya
jitihada ya kuwasaidia Waislamu, jiepushe na kuwasukuma au kuwaumiza
wakati wa kutekeleza Hijjah, hususan wakati kufanya Twawaaf, Sa'y,
kurembea vijiwe, ambapo huwa kuna misongamano mikubwa.
Usafi
Usafi
ni alama ya kweli ya imani. Kwa hivyo, huna budi kuusafisha moyo wako,
kiwiliwili chako, chakula chako, kinywaji chako na kila kitu. Vile vile
wahimize watu wengine kuyafanya matendo na pahala pa ibada kuwa safi
kwa kadiri ya uwezo wao.
Fedha
Usijali kuhusu ubadishaji wa fedha. Unaweza kubadilisha kwa wepesi pahali popote katika miji ya Saudi Arabia.
Vikundi Vidogo Vidogo
Uchunguzi
wa karibu unaonyesha kuwa watu wanaotembea kwenye makundi makubwa huwa
ni rahisi mmoja kati yao au mwengine kupotea, na hii hupelekea kupoteza
au kuchelewa kutenda baadhi ya matendo ya Hijjah ambapo Hujaji hutakiwa
baadae afanye fidia aidha kwa kuchinja mnyama, kufunga au kufanya jambo
jengine.
Fuatana na Watu Wazuri
Hakikisha
unachagua watu wazuri wa kufuatana nao katika nyendo zako zote, hii ni
kwa sababu wataweza kukusaidia kuepukana na mizozo na vile vile
watakusaidia katika kuitekeleza Hijjah yako kwa uhakika
Jiepushe na Kupotea
Inashauriwa
kupanga kwa vizuri na watu unaofuatana nao wapi na ni wakati gani
mkutane na kitu gani cha kufanya pindi mmoja wenu akichelewa kufika au
kupotea. Hatua zifuatazo huenda zikasaidia:
- Panga kukutana pahala pa uwazi, penye alama enye rangi au alama za mji.
-
Ainisha muda maalumu wa kukutana kwa wale watakaochelewa kutokana na
sababu fulani, ukizingatia ya kwamba muda huo hautoathiri vitendo vya
Hijjah vinavyofuata.
- Hakikisha kwamba kila mtu katika kikundi chenu ameelezewa na kufahamu sawasawa.
Chakula
Usichukue
chakula kutoka nchi yako: karibia kila kitu kinapatikana huko. Vile
vile kumbuka kwamba pindi ukichukua chakula huenda ukanyang’anywa kwenye
uwanja wa ndege.
Fuata maelekezo yafuatayo ili uwe na mpangilio mzuri ya kula.
-
Jiepushe na kula chakula kingi, hii ni kwa sababu si katika kujijengea
afya njema na pia haisaidii katika kutekeleza vitendo vya Hijjah.
-
Vyakula bora vya kuliwa ni matunda, na vinywaji bora ni maji na juisi
(juice). Hivi vipo kila pahala na vinauzwa (bei) rahisi.
- Tia chakula kinachobakia (makombo) kwenye mfuko wa plastiki na kisha weka kwenye mapipa ya taka.
Matibabu
Chukua
dawa zile ambazo tu ni muhimu kwa afya yako. Dawa nyengine ambazo ni
maarufu hupatikana katika maduka yoyote ya kuuzia madawa. Unaweza
kupata huduma ya kwanza (first aid) kwenye sehemu zote za ibada.
Hifadhi
Jihadhari
na sehemu zenye joto kali katika sehemu za ibada. Jiepushe kupigwa na
jua kwa muda mrefu. Chukua mwamvuli na vinywaji vya kutosha.
Huduma kwa wasiojiweza
Huduma
maalumu zinapatikana kwa waliodhaifu, wagonjwa, wasiojiweza, na wazee.
Viti na vitanda vya kubebea vinakodishwa kwa wale wanaohitajia. Uliza
wasimamizi wa huduma hizi ndani ya Msikiti. Wakati mwengine huduma hii
hupatikana bure, lakini kwa kawaida hupatikana kwa bei rahisi. Faidika
na huduma hizi pindi ukizihitajia.
No comments:
Post a Comment