Thursday, September 25, 2014

Maajabu Ya Zam Zam



Utafiti wa maji uliofanywa na Tariq Hussain,
Mhandisi wa kutoa chumvi katika maji
Imefasiriwa na Ummu Ummu Ayman

Tumekuja hapa tena kutekeleza Umrah, na nimekumbushwa na maajabu ya Zamzam.
Kisima cha Zamzam ni kisima ambacho Allaah amekichimbua huko Makkah kwa ajili ya mke wa Mtume Ibraahiym na kwa mtoto wake mkubwa Ismail, (amani iwe juu yao wote). Niruhusu nirudi nyuma kuona mambo yalianzaje. Katika mwaka 1971, Daktari wa kimisri aliandika katika European Press, barua inayosema kuwa maji ya Zamzam hayafai kwa matumizi ya kunywa.
Kwa haraka nilifikiria kuwa hii ilikuwa ni aina ya njama dhidi ya Uislam na kuwa kwa kuwa hoja zake ziliegemea katika dhana ya kuwa kwa kuwa Ka’abah ni pahala pafupi (chini ya usawa wa bahari) na ipo katikati ya mji wa Makkah, maji machafu ya mji yanayojikusanya katika mitaro yanaangukia katika kisima cha maji hayo (yaani Zamzam).
Kwa bahati njema, habari hii ilimfika  Mfalme Faysal ambae alikasirika sana na kuamua kupingana na maneno ya uchokozi ya Daktari huyo wa kimisri. Haraka aliamrisha Wizara ya Kilimo na Raslimali ya Maji kuchunguza na kupeleka sampuli za maji ya Zamzam katika maabara za Ulaya kwa ajili ya kuchunguza ubora wa maji hayo.
Wizara baaadae iliielekeza Jeddah Power and Desalination Plants kuifanya kazi hii. Hapo ndipo nilipoajiriwa kama mhandisi wa utoaji wa chumvi majini (mhandisi wa kemikali katika uzalishaji wa maji ya kunywa kutoka katika maji ya chumvi). Nilichaguliwa kuifanya kazi hii.
Kufikia hapo, nakumbuka kuwa sikuwa na fununu yoyote kuhusu kilivyo kisima chenye maji. Nilikwenda Makkah na kuripoti kwa viongozi wa wahusika ili kuelezea madhumuni ya ziara yangu. Walinitengea mtu maalum kunipa msaada wowote ule utaohitajika.
Tulipofika kisimani, ilikuwa vigumu kwa mimi kuamini kuwa, bwawa la maji kama kidimbwi kidogo, kama futi 18 kwa 14, ndio kisima chenye kutoa mamilioni ya magaloni ya maji kila mwaka kwa mahujaji tokea kilipoanza wakati wa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam), karne nyingi zilizopita.
Nilianza uchunguzi wangu na kuchukua vipimo vya kisima hicho. Nilimtaka yule mtu anioenyeshe kina cha kisima hicho. Kwanza alikoga na kuzamia katika maji. Kisha akasimama sawa sawa. Niliona kuwa kina cha maji kimefikia kiasi cha usawa wa mabega yake. Urefu wake ulikuwa  kama futi tano na nchi 8. Kisha akaanza kwenda kutoka kona moja hadi nyengine ndani ya kisima (akiwa amesimama wakati wote kwani hakuruhusiwa kuzamisha kichwa chake ndani ya maji) akijaribu kutafuta paipu inayoingiza maji kisimani ili kuona maji hayo yanakotokea. Hata hivyo, mtu huyo aliripoti kuwa hakuweza kuipata paipu yoyote ndani ya kisima hicho.
Nikapata mawazo mengine. Maji yanaweza kutolewa kwa haraka kwa kutumia pampu kubwa iliyokuwa imewekwa kwa ajili ya kujaza tangi la maji ya Zamzam.  Kwa njia hii, kina cha maji kitapungua na kutuwezesha kupata sehemu yanayoingilia maji. Kwa mshangao, hakuna kilichoonekana wakati wa kuyavuta maji, lakini nilijua kuwa hii ndio njia pekee ya kuweza kuipata sehemu ya kuingilia maji katika kisima. Kwa hivyo niliamua kurejea tena njia hiyo. Lakini mara hii nilimuelekeza yule mtu atulie pahala pamoja na aangalie kwa uangalifu chochote kitachojitokeza ndani ya kisima ambacho si cha kawaida.
Baada ya muda, ghafla alinyanyua mkono wake na kusema kwa nguvu, Alhamdulillah! Nimepaona! Mchanga unacheza cheza chini ya miguu wakati maji yanachimbuka katika sehemu ya chini ya kisima”.
Kisha alikizunguka kisima wakati wa kuvutwa maji na akahisi vile vile katika kila sehemu ya chini ya kisima. Ukweli ni kuwa uchimbukaji wa maji katika kila pahala ulikuwa sawa sawa, kwa hivyo kufanya kina cha maji kiwe kimetulia. Baada ya kumaliza uangalizi wangu nilichukua sampuli za maji kwa ajili ya uchunguzi katika maabara za Ulaya. Kabla ya kuondoka Ka’abah, Niliwauliza wahusika kuhusu visima vyengine vya Makkah. Niliambiwa kuwa visima hivyo karibu vyote vimekauka.
Nilipofika ofisini kwangu Jeddah niliripoti ugunduzi wangu kwa mkuu wangu ambae alinisikiliza kwa hamu kubwa lakini akatoa maoni yake yasiyopendeza kuwa kisima cha Zamzam kumeungana chini kwa chini na Bahari Nyekundu. Itawezekana vipi wakati Makkah iliyo kilomita 75 mbali na bahari, visima vilivyopo kabla ya mji kwa kawaida huwa vikavu.
Matokeo ya sampuli (vielelezo) zilizopimwa katika maabara ya Ulaya na zile ambazo tulizozipima sisi katika maabara yetu yalionekana kuwa karibu ni sawa sawa. Tofauti baina ya maji ya Zamzam na maji ya visima vyengine (maji ya mjini) yalikuwa ni katika viwango vya chumvi za chokaa (calcium) na magnesi (magnesium). Viwango nya chumvi hizi vilikuwa ni vikubwa kidogo katika maji ya Zamzam. Hii inawezekana ikawa ni sababu ya maji haya huwaondoshea uchovu (kuwachangamsha) mahujaji. Lakini kilichojitokeza zaidi, ni kuwa maji hayo yalikuwa na floridi (fluorides) ambayo inaathiri vijidudu.
Zaidi ya hayo, maelezo ya maabara za Ulaya yalionyesha kuwa maji hayo yanafaa kwa kunywa. Kwa hivyo maneno yaliyowekwa na Daktari wa Kimisri yalishuhudiwa kuwa ni ya uongo.
Yaliporipotiwa mambo hayo kwa Mfalme Faysal alifurahi mno na akaamrisha tofauuti za kupingana kati ya ripoti hizo zitolewe katika jarida la European Press.
Kwa njia hiyo, imekuwa ni baraka kuwa uchunguzi huo ulifanyika ili kuonyesha kemikali zilizomo katika maji hayo. Kwa kweli, kadri unavyopekuwa zaidi, ndivyo maajabu yake yanavyojitokeza zaidi na unajikuta mwenyewe unaamini kikamilifu miujiza ya maji hayo ambayo Allaah Amejaalia kuwa zawadi kwa wacha Mungu wanaokuja katika ardhi yenye jangwa kutoka masafa ya mbali kwa ajili ya hija.
Niwache nifupishe baadhi ya maumbile ya maji ya Zamzam
·  Kisima hichi hakijawahi kukauka. Na badili yake daima kimekuwa kinatosheleza mahitaji ya maji.

·  Daima kiwango chake cha chumvi na ladha kinabaki sawa sawa tokea kimekuwepo.

·  Ubora wake kwa kunywa daima  umetambuliwa kimataifa kwa vile mahujaji kutoka duniani kote wamekuwa wakiitembelea Ka’abah kila mwaka kwa ajili ya Hijja na Umra, lakini hakuna alielalamika kuhusu ubora huo. Badili yake, wamekuwa daima wakiyafurahia maji hayo ambayo yanawaondoshea uchovu.

·  Maji huwa na ladha tofauti katika pahala tofauti. Kupendwa kwa maji ya Zamzam kumekuwa ni kwa kimataifa.

·  Maji haya hayajawahi kutibiwa kwa kemikali yoyote au kutiwa klorini kama ilivyo kawaida ya maji yanayopelekwa mijini. Kuota kwa njia ya kibaiolojia (biological growth) vimelea na majani ni kawaida katika visima karibu vyote. Hii inasababisha maji kuwa si mazuri (kwa kunywa) kutokana na kuota kwa mwani (algae) unaoharibu  ladha na harufu. Lakini katika kesi ya kisima cha Zamzam, hakuna dalili yoyote ya kuota kwa vitu hivyo.

·  Karne nyingi zilizopita, Bibi Hajra (‘Alayhas Salaam) alitafuta kwa mfadhaiko maji katika vilima vya Swafaa na Marwa ili kumpa mtoto wake aliekuwa ndio kwanza anazaliwa Nabii Isma’iyl (‘Alayhis Salaam). Alipokuwa anakimbia huku na kule kutafuta maji, mtoto wake alipiga piga miguu yake chini mchangani. Bwawa la maji likachimbuka, kwa rehma za Allaah, yakajifanya kuwa kisima ambacho kimekuja kuitwa Maji ya Zamzam.

No comments:

Post a Comment