Kuchinja - Fadhila, Hikmah Na Hukmu Zake
Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala):
((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))
((Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako)) [Al-Kawthar: 2]
Kuchinja
ni moja ya ibada za Kiislam ambayo inatukumbusha Tawhiyd ya Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) na Baraka Zake kwetu, pamoja na kutupa mafunzo ya
utiifu wa baba yetu Ibraahiym kwa Mola wake na kumpwekesha Allaah.
Hivyo ibada hii ya kuchinja ni muhimu sana kwa Muislam, na inatupasa tuizingatie kwa makini na kuitekeleza.
UBAINIFU WAKE
Ni kuchinja kondoo, ngamia au ng'ombe siku ya 'Iydul-Adhwhaa na siku za Tashriyq (siku ya 11, 12, 13 Dhul-Hijjah) ili kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).
KUWAJIBIKA KWAKE
Kuchinja
ni waajib katika familia ya kila nyumba ya Muislamu, ambayo watu wake
wanao uwezo wa kuchinja. Hii kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa
Ta'ala):
((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))
((Basi Swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako)) [Al-Kawthar: 2]
((وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ))
((Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Allaah; kwa hao mna kheri nyingi)) [Al-Hajj: 36]
Na uthibitisho wa Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
(( ضحى بكبشين أملحين أقرنين ذبحهما بيده وسمى وكبر)) رواه البخاري ومسلم
((Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja kondoo wawili
walionona, walio na pembe, aliwachinja kwa mikono yake akataja jina la
Allaah, Akamtukuza kwa kusema BimiLLaah Allaahu Akbar)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Aliulizwa
Shaykh Muhammad bin 'Uthaymiyn kama masikini inampasa achinje. Akajibu
"Ikiwa anao uwezo wa kuchinja basi achinje ili apate kheri hizi na kama hana uwezo basi haimpasi"
Maoni ya wanachuoni wengi kuhusu Fadhila, Hukmu na Hekima za Hajj ni kama yafuatayo:
FADHILA ZAKE
Kuna
ushahidi kwamba ibada ya kuchinja ina fadhila kubwa kwa sababu ya kauli
ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عن
عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((ما عمل ابن آدم
يوم النحر عملاً أحبُّ إلى الله من إراقة الدم، وإنه ليؤتى يوم القيامة
بقرونها، وأظلافها، وأشعارها، وإن الدم ليقع من الله عز وجل بمكان قبل أن
يقع على الأرض، فطيبوا بها نفساً))
Kutoka
kwa mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu anhaa) kwamba Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna kitendo
cha mwana Adam kilichokuwa ni kipenzi kabisa kwa Allaah siku ya kuchinja
kama kumwaga damu (kuchinja). Atakuja
(huyo mnyama) siku ya Qiyaamah na pembe zake, kucha zake na nywele
zake. Damu yake itamwagika mahali fulani Allaah Anapajua kabla ya
kumwagika katika ardhi. Hivyo zipendezesheni nafsi kwayo)) [At-Tirmidhiy]
HIKMAH YAKE
1. Kujikurubisha Kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama Anavyosema katika kauli Yake:
((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))
((Basi Swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako)) [Al-Kawthar: 2]
Anasema pia:
((قُلْ إِنَّ صَلاَتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ))
(( لاَ شَرِيكَ لَهُ وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَاْ أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ))
((Sema: Hakika Swalah yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Allaah Mola wa viumbe vyote))
((Hana mshirika Wake. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu)) [Al-An'aam: 162-163].
((لَن
يَنَالَ اللَّهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَكِن يَنَالُهُ
التَّقْوَى مِنكُمْ كَذَلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّهَ
عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ))
((Nyama
zao hazimfikii Allaah wala damu zao, lakini unamfikia uchaji
Allaah wenu. Namna hivi Tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Allaah kwa
Alivyokuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema)) [Al-Hajj: 37].
Na kafara ni kuchinja kwa kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
2. Kuihuiisha Sunnah Mojawapo Ya Tawhiyd,
wakati Allaah Alipompa wahyi Ibraahiym (alayhis-salaam) amchinje
mwanawe Ismaa'iyl. Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akampa fidia ya
kondoo, akamchinja badala yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
((وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ))
((Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu)) [Aswaaffaat: 107]
3. Muislam Kuweza Kuwalisha Nyama Familia Yake Pamoja Na Jamaa Zake Siku Ya 'Iyd na kueneza Rahma miongoni mwa masikini na mafakiri.
4. Kutoa Shukurani Kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kutujaalia kuwa na wanyama wafugwao kama Anavyosema:
((وَالْبُدْنَ
جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ
فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا
فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ كَذَلِكَ
سَخَّرْنَاهَا لَكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ))
((
لَن يَنَالَ اللَّهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَكِن يَنَالُهُ
التَّقْوَى مِنكُمْ كَذَلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّهَ
عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ))
((Na
ngamia wa sadaka Tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa
Allaah; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Allaah juu yao
wanaposimama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na
walisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba. Ndio kama hivi Tumewafanya
hawa wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru))
((Nyama
zao hazimfikii Allaah wala damu zao, lakini unamfikia uchaji
Allaah wenu. Namna hivi Tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Allaah kwa
Alivyokuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema)) [Al-Hajj: 36-37]
HUKMU ZAKE
Umri Wake:
Kondoo
wawe ni kondoo jike ambao wamekamilisha umri wa mwaka mmoja takriban.
Mbuzi wawe wamekamilisha umri wa mwaka mmoja na kuingia mwaka wa pili.
Ngamia wawe wamekamilisha umri wa miaka minne na kuingia wa tano.
Ng'ombe wawe wamekamilisha miaka miwili na kuingia mwaka wa tatu, kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((لا تذبحوا إلا مسنة إلا أن تعسر عليكم فتذبحوا جذعة من الضأن)) رواه مسلم
((Msichinjie
ila mnyama mwenye makamo isipokuwa ikiwa ni shida kwenu, hivyo mchinje
kondoo (japo wa chini ya umri wa mwaka lakini awe zaidi ya umri wa miezi
sita)) [Muslim]
Usalama Wake:
Asiwe na kasoro yoyote kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((أربع لا تجوز في الأضاحي: العوراء البيّن عورها، والمريضة البيّن مرضها، والعرجاء البيّن ظلعها ، والعجفاء التي لا تنقي))
((Mambo
manne (kasoro nne) hayapasi katika kuchinja; mwenye jicho chongo lenye
kudhihirika, mnyama mgonjwa mwenye kudhihirika ugonjwa wake, kilema
mwenye kudhihirika kuchechemea kwake na aliyedhoofika ambaye hana nyama
katika mifupa yake)) [Swahiyh Al-Jaami']
Wakati Wa Kuchinja:
Kuchinja
asubuhi ya siku ya 'Iyd baada ya Swalah. Hairuhusiwi kuchinja kabla ya
Swalah kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam):
حديث أنس رضي الله عنه- قال: قال رسول الله -صلى الله عليه وسلم ((من ذبح قبل الصلاة فإنما ذبح لنفسه، ومن ذبح بعد الصلاة فقد تم نسكه وأصاب سنة المسلمين)) البخاري ومسلم
Kutoka
kwa Anas (Radhiya Allaahu 'anhu kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayechinja kabla ya Swalah atakuwa
amejichinjia kwa ajili yake mwenyewe. Na Atakayechinja baada ya Swalah
atakamilisha kafara (kichinjo) yake na atapata (atatekeleza) Sunnah ya
Waislam)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Anaweza kuchinja siku ya pili ya 'Iyd au kuchelewesha hadi siku ya mwisho ya Ayyaamut-Tashriyq (siku za Tashriyq) ambayo ni siku ya kumi na tatu Dhul-Hijjah.
(... وفي كل أيام التشريق ذبح))
((...siku zote za Tashriyq ni siku za kuchinja)) [Ahmad]
YANAYOPENDEKEZEKA KATIKA KUCHINJA
Kumpwekesha Allaah:
Inapendekezeka kumuelekeza mnyama Qiblah wakati wa kumchinja na kusoma:
((إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ حَنِيفًا وَمَا أَنَاْ مِنَ الْمُشْرِكِينَ))
((Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa Aliyeziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina))[Al-An'aam:79]
((إِنَّ صَلاَتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ)) ((لاَ شَرِيكَ لَهُ وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَاْ أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ))
((Hakika Swalah yangu, na kichinjo changu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Allaah, Mola wa viumbe vyote))
((Hana mshirika Wake. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu)) [Al-An'aam: 162-163].
Anapoanza Kuchinja Aseme:
((بسم الله والله اكبر، اللهم هذا منك ولك))
((BismiLLaah, wa Allaahu Akbar, Ewe Allaah hii ni kutoka Kwako na kwa ajili Yako))
Kuchinja mwenyewe ni bora zaidi:
Inapendekezeka
Muislamu achinje mwenyewe na akimuwakilisha mtu kumchinjia pia
inaruhusiwa hakuna ikhtilaaf katika jambo hili baina ya Maulamaa.
KUGAWA NYAMA
Inapendekeza
kuigawa nyama sehemu tatu. Ya kwanza wale familia yake, sehemu ya pili
kugawa sadaqah na sehemu ya tatu kuwagawia marafiki, jirani n.k. kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((لِيَشْهَدُوا
مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ
عَلَى مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ فَكُلُوا مِنْهَا
وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ))
((Ili washuhudie manufaa yao
na walitaje jina la Allaah katika siku maalumu juu ya nyama hao
Aliowaruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye
fakiri)) [Al-Hajj: 28]
((وَالْبُدْنَ
جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ
فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا
فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ))
((Na
ngamia wa sadaka Tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa
Allaah, kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Allaah juu yao wanaposimama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na walisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba)) [al-Hajj: 36]
Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
((كلوا وأطعموا وادخروا)). رواه البخاري
((Kuleni, lisheni na mbakishe [akiba])) [Al-Bukhaariy]
Na usemi mwengine kutoka kwa Muslim kutoka kwa mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa)
عن عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلّم قال: ((كلوا وادخروا وتصدقوا)) رواه مسلم.
((Kuleni, bakisheni na mtoe sadaka)) [Muslim]
Inaruhusiwa pia kuigawa nyama yote sadaqah na Inaruhusiwa kubakisha sehemu.
HAIFAI KUMPA CHOCHOTE KATIKA NYAMA MCHINJAJI KAMA UJIRA
Hairuhusiwi kumlipa mchinjaji aliyewakilishwa kuchinja baadhi ya nyama kama ujira wake kutokana na Hadiyth ifuatayo:
عن علي قال: أمرني رسول الله صلى الله عليه وسلم أن أقوم على بدنه وأن أتصدق بلحومها وجلدها وأجلتها (وأجلتها: أي لباسها الذي يقيها البرد. ) وأن لا أعطي الجزار منها شيئا، وقال: نعطيه من عندنا.
Kutoka
kwa 'Aliy (Radhiya Alalhu 'anhu):"Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) aliniamrisha kuchinja? Na kutoa nyama, ngozi na kile
kinachomfunika kumhifadhi na baridi kuvitolea sadaqah na nisimpe
chochote katika nyama hiyo. ((Tutampa kitu tulichonacho)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ufafanuzi Zaidi:
Ukichinja AL-HADYI, mchinjaji hapewi katika nyama alioichinja lakini anapewa ujira wake. AL-HADYI ni kuchinja na wewe upo katika Hajj.
Ukichinja UDHWHIYAH, mchinjaji anaweza akapewa katika nyama hiyo aliyoichinja kama sadaka ikiwa ni masikini, na atapewa pamoja na ujira wake. UDHWHIYAH ni kichinjo kwa wale wasiokuwa katika Hajj. Walio katika Hajj kichinjo kinaitwa AL-HADYI.
MNYAMA MMOJA ANATOSHELEZA FAMILIA NZIMA
Kuchinja mnyama mmoja anatosheleza katika kila familia japo kama kuna watu wengi katika familia kutokana na kauli ya:
أبي أيوب -رضي الله عنه- لما سئل: كيف كانت الضحايا على عهد رسول الله؟ فقال: "كان الرجل يضحي بالشاة عنه وعن أهل بيته" (الترمذي)
Abu
Ayyuub (Radhiya Allaahu 'anhu) alipoulizwa: "Uchinjaji ulikuwa vipi zama
za Mjumbe wa Allaah?" Akajibu: "Mtu alikuwa anachinja kondoo mmoja kwa
ajili yake na familia yake" [At-Trimidhiy]
YANAYOMPASA KUFANYA MWENYE KUTAKA KUCHINJA
Baada ya kutia Niya ya kuchinja, asikate mtu nywele wala kucha mpaka amalize kuchinja kama tulivyoamrishwa katika Hadiyth ifuatayo:
عن أم سلمة رضي الله عنها، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: (( إذا رأيتم هلال ذي الحجة وأراد أحدكـم أن يضحّي فليمسك عــن شعره وأظفاره)) ، وفي راوية (( فلا يأخذ من شعره ولا من أظفـاره حتى يضحّي )) مسلم
Imetoka kwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ukiandama mwezi wa Dhul-Hijjah na ikiwa yuko anayetaka kuchinja basi azuie (asikate) nywele zake na kucha zake))
Na katika riwaya nyingine ((Asikate nywele wala kucha mpaka atakapomaliza kuchinja)) [Muslim na wengineo]
MWENYE UWEZO WA KUCHINJA ZAIDI YA MMOJA
Mwenye uwezo wa kuchinja zaidi ya mmoja na akipenda achinje kama
alivyochinja Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa
ajili ya Ummah wa Kiislam wote. Hivyo Muislam asiye na uwezo wa kuchinja
naye atapata fadhila hizi za kuchinja, naye mchinjaji atachuma thawabu
za Waislam wote wasio na uwezo. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam) alifanya hivyo:
وعن أبي رافع رضي الله عنه «أن النبي صلىالله عليه وسلّم كان يضحي بكبشين أحدهما عنه وعن آله، والاخر عن أمته جميعاً»، رواه أحمد
Kutoka
ka Abu Raafi' (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba: Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akichinja kondoo wawili; mmoja kwa
ajili yake na familia yake na wa mwengine kwa ajili ya Ummah wake wote)) [Ahmad]
Kutoka kwa Jaabir kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akichinja kwa ajili ya Ummah akisema:
(( بسم الله والله أكبر. اللهم هذا عني وعمن لم يضح من أمتي)) رواه أحمد وأبو داود والترمذي.
((BismiLLaah, wa Allaahu Akbar, Ee Allaah hii kwa ajili yangu na kwa ajili ya wasio na uwezo katika Ummah wangu)) [Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy]
No comments:
Post a Comment